Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 29:1-13

Kumbukumbu 29:1-13 NENO

Haya ndio maneno ya agano Mwenyezi Mungu alilomwagiza Musa kufanya na Waisraeli huko Moabu, yakiwa nyongeza ya agano alilofanya nao huko Horebu. Musa akawaita Waisraeli wote, akawaambia: Macho yenu yameona yale yote Mwenyezi Mungu aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote. Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa. Lakini hadi leo Mwenyezi Mungu hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia. Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda. Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao. Zingatieni masharti ya agano hili, ili mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya. Ninyi nyote leo mnasimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli, pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni wanaoishi katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji. Mnasimama hapa ili kufanya agano na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo, kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Ibrahimu, Isaka na Yakobo.