Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 4

4
Umoja katika mwili wa Al-Masihi
1Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana Isa, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3Jitahidini kudumisha umoja wa Roho wa Mungu katika kifungo cha amani. 4Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. 5Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo#4:5 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao. mmoja, 6Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.
7Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Al-Masihi. 8Kwa hiyo husema:
“Alipopaa juu zaidi,
aliteka mateka,
akawapa wanadamu vipawa.”#4:8 Zaburi 68:18
9(Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema kwamba Al-Masihi pia alishuka pande za chini sana za dunia#4:9 pande za chini sana za dunia hapa maana yake Kuzimu? 10Yeye aliyeshuka ndiye aliyepaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.) 11Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili mwili wa Al-Masihi upate kujengwa 13hadi sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua Mwana wa Mungu#4:13 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. na kuwa watu wazima, kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Al-Masihi.
14Basi hatutakuwa tena watoto wachanga, tukiyumbishwa na mawimbi, na tukipeperushwa hapa na pale na kila upepo wa mafundisho, na kwa ujanja na hila za watu katika njama zao. 15Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani Al-Masihi. 16Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, huku kila kiungo kikifanya kazi yake.
Maisha ya zamani na maisha mapya
17Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana Isa kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa wanavyoishi, katika ubatili wa mawazo yao. 18Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kujiingiza katika kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.
20Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Al-Masihi. 21Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Isa. 22Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23ili mfanywe upya katika roho ya nia zenu, 24na mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki ya kweli na utakatifu.
Kanuni za maisha mapya
25Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26Mkikasirika, msitende dhambi,#4:26 Zaburi 4:4 wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27wala msimpe ibilisi nafasi. 28Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kinachofaa kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.
29Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yanayofaa kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu na hasira, makelele na masingizio, pamoja na kila aina ya uovu. 32Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Al-Masihi alivyowasamehe ninyi.

Iliyochaguliwa sasa

Waefeso 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia