Kutoka 14:1-9
Kutoka 14:1-9 NEN
Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni. Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’ Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi BWANA.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo. Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!” Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake. Akachukua magari bora mia sita, pamoja na magari mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote. BWANA akaufanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri. Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.