Kutoka 16:9-26
Kutoka 16:9-26 NENO
Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia manung’uniko yenu.’ ” Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Mwenyezi Mungu ukitokeza katika wingu. Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nimesikia manung’uniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ” Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi. Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Mwenyezi Mungu amewapa mle. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji. Kisha Musa akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote hadi asubuhi.” Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Musa, wakahifadhi kiasi fulani hadi asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Musa akawakasirikia. Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Musa. Musa akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Kesho itakuwa Sabato ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke hadi asubuhi.’ ” Kwa hiyo wakavihifadhi hadi asubuhi, kama Musa alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. Musa akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwa chochote.”