Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 17:1-7

Kutoka 17:1-7 NENO

Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. Kwa hiyo wakagombana na Musa wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Musa akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Mwenyezi Mungu?” Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanung’unika dhidi ya Musa, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?” Kisha Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.” Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Nenda mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, na uchukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Musa akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. Naye akapaita mahali pale Masa na Meriba, kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Mwenyezi Mungu wakisema, “Je, Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi au la?”