Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 24

24
Agano lathibitishwa
1Kisha Mungu akamwambia Musa, “Njooni huku juu kwa Mwenyezi Mungu, wewe na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, 2lakini Musa peke yake ndiye atakayemkaribia Mwenyezi Mungu; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.”
3Musa alipoenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Mwenyezi Mungu, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu tutakifanya.” 4Ndipo Musa akaandika kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amesema.
Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. 5Kisha akawatuma vijana wanaume Waisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu. 6Musa akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli, na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. 7Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu, nasi tutatii.”
8Ndipo Musa akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
9Musa na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. 11Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.
12Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.”
13Basi Musa akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Musa akapanda juu kwenye mlima wa Mungu. 14Musa akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa hadi tutakapowarudia. Haruni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na shauri aweza kuwaendea wao.”
15Musa alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima, 16nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba Mwenyezi Mungu akamwita Musa kutoka kati ya lile wingu. 17Kwa Waisraeli utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima. 18Kisha Musa akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia