Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 8:1-15

Kutoka 8:1-15 NEN

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura. Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga. Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ” Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ” Ndipo Aroni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi. Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri. Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kusema, “Mwombeni BWANA awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea BWANA dhabihu.” Mose akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako na watu wako ili kwamba vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu. Isipokuwa wale walio katika Mto Naili.” Farao akasema, “Kesho.” Mose akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama BWANA Mungu wetu. Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.” Baada ya Mose na Aroni kuondoka kwa Farao, Mose akamlilia BWANA kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao. Naye BWANA akafanya lile Mose alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani. Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka. Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema.