Kutoka 9:27-35
Kutoka 9:27-35 NEN
Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. BWANA ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji. Mwombeni BWANA, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kututosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.” Mose akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba BWANA. Ngurumo zitakoma na hapatakuwepo mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa, nchi ni mali ya BWANA. Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi BWANA Mungu.” (Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa katika kutoa maua. Hata hivyo, ngano na jamii nyingine ya ngano hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa bado.) Kisha Mose akaondoka kwa Farao akaenda nje ya mji. Mose akanyoosha mikono yake kuelekea kwa BWANA, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini. Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu. Kwa hiyo moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile BWANA alivyokuwa amesema kupitia Mose.