Ezekieli 16:44-63
Ezekieli 16:44-63 NENO
“ ‘Kila mtu anayetumia mithali atatumia mithali hii kukuhusu: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.” Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimdharau mume wake na watoto wake; tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowadharau waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako alikuwa Mwamori. Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake; naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini mwako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma. Hukuenda katika njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali baada ya muda mfupi, ulipotoka zaidi yao katika njia zako zote Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya. “ ‘Sasa hii ndiyo ilikuwa dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa wenye kujigamba, walafi na wasiojali; hawakuwasaidia maskini na wahitaji. Walijivuna na kufanya mambo ya kuchukiza sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona. Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya. Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi yako. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki. “ ‘Lakini nitarudisha baraka za Sodoma na binti zake na za Samaria na binti zake, nami nitarudisha baraka zako pamoja na zao, ili upate kuchukua aibu yako na kufedheheka kwa ajili ya yote uliyotenda ambayo yamekuwa faraja kwao wakijilinganisha na wewe. Nao dada zako, Sodoma na binti zake na Samaria na binti zake, watarudishwa kama vile walivyokuwa mwanzoni, nawe pamoja na binti zako mtarudishwa kama mlivyokuwa hapo awali. Hukuweza hata kumtaja dada yako Sodoma kwa sababu ya dharau yako katika siku za kiburi chako, kabla uovu wako haujafunuliwa. Hata hivyo, sasa unadhihakiwa na binti za Shamu na majirani zake wote, na binti za Wafilisti, wale wote wanaokuzunguka wanakudharau. Utachukua matokeo ya uasherati wako na matendo yako ya kuchukiza, asema Mwenyezi Mungu. “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakutendea kama unavyostahili, kwa kuwa umedharau kiapo changu kwa kuvunja agano. Lakini nitakumbuka agano nililolifanya nawe wakati wa ujana wako, nami nitaweka nawe agano imara la milele. Ndipo utakapozikumbuka njia zako na kuona aibu utakapowapokea dada zako, wale walio wakubwa wako na wadogo wako. Nitakupa hao wawe binti zako, lakini si katika msingi wa agano langu na wewe. Hivyo nitalifanya imara agano langu na wewe, nawe utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Basi, nitakapofanya upatanisho kwa ajili yako, kwa yale yote uliyoyatenda, utakumbuka na kuaibika, nawe kamwe hutafumbua tena kinywa chako kwa sababu ya aibu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”