16
Yerusalemu mwanamke asiye mwaminifu
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, kabili Yerusalemu kuhusu matendo yake ya kuchukiza, 3useme, ‘Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Asili na kuzaliwa kwako kulikuwa ni katika nchi ya Wakanaani; baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti. 4Siku uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo. 5Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa.
6“ ‘Nami nikapita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!” 7Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote.
8“ ‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, niliutandaza upindo wa vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye agano na wewe, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nawe ukawa wangu.
9“ ‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta. 10Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa. 11Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako, 12nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako. 13Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; nguo zako zilikuwa za kitani safi, na hariri, na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana, ukainuka kuwa malkia. 14Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
15“ ‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uasherati na kila mtu aliyepita, nao uzuri wako ukawa wake. 16Ulichukua baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia, ambapo uliendeleza ukahaba wako. Mambo kama hayo hayastahili kutendeka wala kamwe kufanyika. 17Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo. 18Ukayachukua mavazi yako yaliyotariziwa, na kuyavalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu. 19Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
20“ ‘Nawe uliwachukua wanao wa kiume na wa kike ulionizalia na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha? 21Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu. 22Katika matendo yako yote ya machukizo pamoja na ukahaba wako, hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako.
23“ ‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mungu Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine, 24Ulijijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za sanamu kwenye kila uwanja wa mikutano. 25Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za sanamu, na kuuaibisha uzuri wako, ukizidi kuutoa mwili wako kwa uzinzi kwa kila apitaye. 26Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, majirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako. 27Hivyo niliunyoosha mkono wangu dhidi yako na kuipunguza nchi yako; nikakutia kwenye ulafi wa adui zako, binti za Wafilisti, walioshtushwa na tabia yako ya uasherati. 28Ulifanya ukahaba na Waashuru pia, kwa kuwa hukuridhika, hata baada ya hayo, ukawa bado hukutosheleka. 29Ndipo uliuzidisha uzinzi wako kwa kujumuisha Ukaldayo, nchi ya wafanyabiashara; lakini hata katika hili hukutosheka.
30“ ‘Tazama jinsi ulivyo na dhamiri dhaifu, asema Bwana Mungu Mwenyezi, unapofanya mambo haya yote, unatenda kama kahaba asiye aibu! 31Ulipojenga jukwaa lako katika mwanzo wa kila barabara, na kutengeneza mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu katika kila kiwanja cha wazi, hukuwa kama kahaba, kwa sababu ulidharau malipo.
32“ ‘Wewe mke mzinzi! Unapenda wageni, kuliko mume wako mwenyewe. 33Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako. 34Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako. Hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, bali wewe ulikuwa tofauti kabisa, kwani ulilipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe.
35“ ‘Kwa hiyo, wewe kahaba, sikia neno la Mwenyezi Mungu! 36Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa umemwaga tamaa zako na kuonesha uchi wako katika uzinzi wako kwa wapenzi wako na kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo na kwa sababu uliwapa damu ya watoto wako, 37kwa hiyo nitawakusanya wapenzi wako wote, wale uliojifurahisha nao: wale uliowapenda kadhalika na wale uliowachukia. Nitawakusanya wote dhidi yako kutoka pande zote, na nitakuvua nguo mbele yao, nao wataona uchi wako wote. 38Nitakuhukumia adhabu wanayopewa wanawake wafanyao uasherati na hao wanaomwaga damu; nitaleta juu yako kisasi cha damu cha ghadhabu yangu na hasira yangu yenye wivu. 39Kisha nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa majukwaa yako na kuharibu mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu. Watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vya thamani na kukuacha uchi na bila kitu. 40Wataleta kundi la watu dhidi yako, watakaokupiga kwa mawe na kukukatakata vipande vipande kwa panga zao. 41Watachoma nyumba zako na kutekeleza adhabu juu yako machoni pa wanawake wengi. Nitakomesha ukahaba wako, nawe hutawalipa tena wapenzi wako. 42Ndipo ghadhabu yangu dhidi yako itapungua, na hasira yangu yenye wivu itakuondokea. Nitatulia, wala sitakasirika tena.
43“ ‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinighadhibisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Je, hukuongeza uasherati juu ya matendo yako mengine ya kuchukiza?
44“ ‘Kila mtu anayetumia mithali atatumia mithali hii kukuhusu: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.” 45Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimdharau mume wake na watoto wake; tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowadharau waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako alikuwa Mwamori. 46Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake; naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini mwako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma. 47Hukuenda katika njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali baada ya muda mfupi, ulipotoka zaidi yao katika njia zako zote 48Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.
49“ ‘Sasa hii ndiyo ilikuwa dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa wenye kujigamba, walafi na wasiojali; hawakuwasaidia maskini na wahitaji. 50Walijivuna na kufanya mambo ya kuchukiza sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona. 51Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya. 52Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi yako. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki.
53“ ‘Lakini nitarudisha baraka za Sodoma na binti zake na za Samaria na binti zake, nami nitarudisha baraka zako pamoja na zao, 54ili upate kuchukua aibu yako na kufedheheka kwa ajili ya yote uliyotenda ambayo yamekuwa faraja kwao wakijilinganisha na wewe. 55Nao dada zako, Sodoma na binti zake na Samaria na binti zake, watarudishwa kama vile walivyokuwa mwanzoni, nawe pamoja na binti zako mtarudishwa kama mlivyokuwa hapo awali. 56Hukuweza hata kumtaja dada yako Sodoma kwa sababu ya dharau yako katika siku za kiburi chako, 57kabla uovu wako haujafunuliwa. Hata hivyo, sasa unadhihakiwa na binti za Shamu na majirani zake wote, na binti za Wafilisti, wale wote wanaokuzunguka wanakudharau. 58Utachukua matokeo ya uasherati wako na matendo yako ya kuchukiza, asema Mwenyezi Mungu.
59“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakutendea kama unavyostahili, kwa kuwa umedharau kiapo changu kwa kuvunja agano. 60Lakini nitakumbuka agano nililolifanya nawe wakati wa ujana wako, nami nitaweka nawe agano imara la milele. 61Ndipo utakapozikumbuka njia zako na kuona aibu utakapowapokea dada zako, wale walio wakubwa wako na wadogo wako. Nitakupa hao wawe binti zako, lakini si katika msingi wa agano langu na wewe. 62Hivyo nitalifanya imara agano langu na wewe, nawe utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 63Basi, nitakapofanya upatanisho kwa ajili yako, kwa yale yote uliyoyatenda, utakumbuka na kuaibika, nawe kamwe hutafumbua tena kinywa chako kwa sababu ya aibu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”