Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:18-32

Ezekieli 20:18-32 NEN

Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, fuateni amri zangu tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu. Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” “ ‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani. Lakini nikauzuia mkono wangu na kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kingelifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba ningewatawanya miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, kwa sababu hawakutii sheria zangu lakini walikuwa wamekataa amri zangu na kuzinajisi Sabato zangu, nayo macho yao yakatamani sanamu za baba zao. Pia niliwaacha wafuate amri ambazo hazikuwa nzuri na sheria ambazo mtu hawezi kuishi kwa hizo sheria. Nikawaacha wanajisiwe kwa matoleo yao, kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu, yaani, kule kuwapitisha wazaliwa wao wa kwanza kwenye moto, nipate kuwajaza na hofu ili wajue kwamba Mimi ndimi BWANA.’ “Kwa hiyo, mwanadamu, sema na watu wa Israeli na uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Katika hili pia, baba zenu walinikufuru kwa kuniacha mimi: Nilipowaleta katika nchi ile ambayo nilikuwa nimeapa kuwapa na kuona kilima chochote kirefu au mti wowote wenye majani mengi, huko walitoa dhabihu zao, wakatoa sadaka ambazo zilichochea hasira yangu, wakafukiza uvumba wenye harufu nzuri na kumimina sadaka zao za kinywaji. Ndipo nikawaambia: Ni nini maana yake hapa mahali pa juu pa kuabudia miungu mnapopaendea?’ ” (Basi jina la mahali pale panaitwa Bama hata hivi leo.) “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Je, mtajinajisi kama vile baba zenu walivyofanya na kutamani vinyago vyao vya machukizo? Mnapotoa matoleo yenu, yaani, wana wenu kafara katika moto, mnaendelea kujinajisi na sanamu zenu zote hadi siku hii ya leo. Je, niulizwe neno na ninyi, ee nyumba ya Israeli? Hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, mimi sitaulizwa neno na ninyi. “ ‘Lile lililoko mioyoni mwenu kamwe halitatokea, mnaposema, “Tunataka tuwe kama mataifa mengine, kama watu wengine wa dunia, wanaotumikia miti na mawe.”