Ezekieli 21:18-32
Ezekieli 21:18-32 NEN
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini. Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome. Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama. Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka vyombo vya kuvunjia boma, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka vyombo vya kuvunjia boma kwenye malango, kuweka jeshi kuzunguka na kufanya uzingiraji. Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha juu ya uovu wao na kuwachukua mateka. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu enyi watu mmekumbusha uovu wenu kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mfanyayo, kwa kuwa mmefanya jambo hili, mtachukuliwa mateka. “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yako imewadia, ambaye wakati wako wa adhabu umefikia kilele chake, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa na aliyekwezwa atashushwa. Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya mpaka aje yule ambaye ndiye mwenye haki nao; yeye ndiye nitakayempa.’ “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo kuhusu Waamoni na matukano yao. “ ‘Upanga, upanga, umefutwa kwa ajili ya kuua, umesuguliwa ili kuangamiza na unametameta kama umeme wa radi! Wakati wakitoa maono ya uongo kwa ajili yako, wanapobashiri uongo kwa ajili yako, wanakuweka wewe kwenye shingo za watu wapotovu, wale walio waovu, wale ambao siku yao imewadia, wakati wa adhabu yao ya mwisho. Urudishe upanga kwenye ala yake! Katika mahali ulipoumbiwa, katika nchi ya baba zako, huko nitakuhukumu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako; nitakutia mikononi mwa watu wakatili, watu stadi katika kuangamiza. Mtakuwa kuni za kuwashia moto, damu yenu itamwagwa katika nchi yenu, wala hamtakumbukwa tena; kwa maana Mimi BWANA nimesema.’ ”