Ezekieli 22:1-16
Ezekieli 22:1-16 NEN
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji umwagao damu? Basi uujulishe juu ya matendo yake yote ya machukizo uuambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ee mji ule ujileteao maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, Ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia. “ ‘Ona jinsi kila mkuu wa Israeli aliyeko ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane. Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za miungu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa si safi. Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti wa baba yake hasa. Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema BWANA Mwenyezi. “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi BWANA nimesema na nitalifanya. Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. Ukiisha kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”