Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 43:13-27

Ezekieli 43:13-27 NEN

“Hivi ndivyo vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ndefu, yaani, dhiraa moja na nyanda nne: Tako lake liwe na kina cha hiyo dhiraa moja na upana wa hiyo dhiraa moja, ikiwa na ukingo wa shibiri moja kuizunguka pembeni. Hiki kitakuwa ndicho kimo cha madhabahu: Kimo cha msingi kuanzia usawa wa ardhi mpaka kwenye mfereji sehemu ya chini kimo chake ni dhiraa mbili na upana wake ni dhiraa moja na kuanzia kwenye ukingo mdogo hadi kwenye ukingo mpana kimo chake ni dhiraa nne na upana wake ni dhiraa moja. Pale pawashwapo moto madhabahuni kimo chake kitakuwa dhiraa nne, na pembe nne zinazoelekeza juu kutoka pale pawashwapo moto. Pale pawashwapo moto pa madhabahu ni mraba, urefu wake ni dhiraa kumi na mbili na upana wa dhiraa kumi na mbili. Pia sehemu ya juu ni mraba, urefu wake dhiraa kumi na nne na upana wa dhiraa kumi na nne, ikiwa na ukingo wa nusu dhiraa na mfereji kuizunguka madhabahu. Ngazi za kupandia madhabahuni zitaelekea upande wa mashariki.” Kisha akaniambia, “Mwanadamu, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Haya ndiyo yatakayokuwa masharti ya kutoa dhabihu za kuteketezwa na kunyunyiza damu juu ya madhabahu itakapokuwa imejengwa. Utatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi kwa makuhani, ambao ni Walawi, wa jamaa ya Sadoki, ndio watakaonikaribia kuhudumu mbele zangu, asema BWANA Mwenyezi. Itakupasa kuchukua baadhi ya hiyo damu ya mnyama huyo na kuiweka juu ya hizo pembe nne za madhabahu na juu ya ncha zake nne za sehemu ya juu kuzunguka ukingo wote, ili kuitakasa madhabahu na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Itakupasa kumchukua huyo fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kumteketeza mahali palipoagizwa katika eneo la Hekalu nje ya mahali Patakatifu. “Siku ya pili yake utamtoa beberu asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nayo madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa yule fahali. Utakapokuwa umemaliza kazi ya kuitakasa, utamtoa fahali mchanga pamoja na kondoo dume toka kwenye kundi, wote wawe hawana dosari. Utawatoa mbele za BWANA, nao makuhani watanyunyizia chumvi juu yao na kuwatoa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. “Kwa siku saba itakupasa kutoa beberu kila siku kwa ajili ya sadaka ya dhambi, pia itakupasa kutoa fahali mchanga na kondoo dume kutoka zizini, wote wawe hawana dosari. Kwa siku saba itawapasa kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuitakasa na hivyo ndivyo watakavyoiweka wakfu. Mwishoni mwa hizi siku saba, kuanzia siku ya nane na kuendelea, itawapasa makuhani kutoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu. Kisha nitawakubali ninyi, asema BWANA Mwenyezi.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezekieli 43:13-27