1
Salamu
1Paulo mtume, si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Isa Al-Masihi na Mungu Baba#1:1 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi aliyemfufua Isa kutoka kwa wafu, 2na ndugu wote walio pamoja nami.
Kwa makundi ya waumini wa Galatia.
3Neema na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi, 4yeye aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu. 5Utukufu una yeye milele na milele. Amen.
Hakuna Injili nyingine
6Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Al-Masihi na kuifuata Injili nyingine, 7ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Al-Masihi. 8Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!
10Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Al-Masihi.
Paulo ameitwa na Mwenyezi Mungu
11Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. 12Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Isa Al-Masihi.
13Ninyi mmekwisha kusikia kuhusu maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyotesa makundi ya waumini wa Mungu kwa nguvu na kujaribu kuwaangamiza. 14Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika langu, maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. 15Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, 16alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, 17wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilienda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.
18Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa#1:18 yaani Petro na nilikaa naye siku kumi na tano. 19Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana Isa. 20Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo.
21Baadaye nilienda sehemu za Siria na Kilikia. 22Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makundi ya waumini huko Yudea yaliyo katika Al-Masihi. 23Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo awali alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.” 24Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.