Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 18:1-15

Mwanzo 18:1-15 NEN

BWANA akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. Abrahamu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi. Akasema, “Kama nimepata kibali machoni penu, ee bwana wangu, usimpite mtumishi wako. Acha yaletwe maji kidogo, kisha ninyi nyote mnawe miguu yenu na mpumzike chini ya mti huu. Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.” Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.” Hivyo Abrahamu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.” Kisha Abrahamu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti. Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?” Akasema, “Yuko huko, ndani ya hema.” Kisha BWANA akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.” Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake. Abrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?” Ndipo BWANA akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa BWANA? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.” Sara akaogopa kwa kuwa alidanganya na kusema, “Mimi sikucheka.” Lakini Bwana akasema, “Ndiyo, ulicheka!”