Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 19:1-11

Mwanzo 19:1-11 NENO

Malaika wale wawili walifika Sodoma wakati wa jioni, naye Lutu alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Alipowaona, alienda kuwalaki, akasujudu, uso wake ukagusa chini. Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa, kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.” Wakamjibu, “La, tutalala hapa uwanjani.” Lakini aliwasihi sana hadi wakaingia nyumbani mwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala. Kabla hawajaenda kulala, wanaume wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba. Wakamwita Lutu wakisema, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuwalawiti.” Lutu akatoka nje kuongea nao, akaufunga mlango nyuma yake. Akawaambia, “La hasha, rafiki zangu! Msifanye jambo hili ovu. Tazama, ninao binti zangu wawili ambao ni bikira. Acha niwatoe kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote wanaume hawa, kwa sababu wako chini ya ulinzi wa dari langu.” Wakamjibu, “Tuondokee mbali!” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Lutu na kuusogelea mlango ili kuuvunja. Lakini wanaume wale waliokuwa ndani wakanyoosha mikono yao, wakamvuta Lutu ndani ya nyumba na kuufunga mlango. Kisha wakawapiga kwa upofu wale wanaume waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.