Mwanzo 2:18-25
Mwanzo 2:18-25 NEN
BWANA Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” Basi BWANA Mungu alikuwa ametengeneza kutoka ardhi wanyama pori wote, na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa jina lake. Hivyo Adamu akawapa majina mifugo wote, ndege wa angani, na wanyama pori wote. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. Hivyo BWANA Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. Kisha BWANA Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwa ule ubavu alioutoa kwa mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa mwanaume. Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke’, kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.” Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Adamu na mkewe wote walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.



