Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 38

38
Yuda na Tamari
1Wakati ule, Yuda akawaacha ndugu zake, akaenda kuishi na Hira Mwadulami. 2Huko Yuda akakutana na binti ya Mkanaani aitwaye Shua. Akamwoa na akakutana naye kimwili, 3naye akapata mimba, na akamzaa mwana, aliyeitwa jina Eri. 4Akapata mimba tena, akamzaa mwana na kumwita jina Onani. 5Akamzaa mwana mwingine tena, akamwita jina Shela. Huyu alimzalia huko Kezibu.
6Yuda akamtwalia Eri, mzaliwa wake wa kwanza, mke aliyeitwa Tamari. 7Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamuua.
8Kisha Yuda akamwambia Onani, “Kutana kimwili na mke wa ndugu yako, na utimize wajibu wako kwake kama mke wa ndugu yako, ili umpatie ndugu yako uzao.” 9Lakini Onani alijua kwamba uzao haungekuwa wake, kwa hiyo kila alipokutana kimwili na mke wa ndugu yake, alimwaga mbegu chini ili asimpatie ndugu yake uzao. 10Alichofanya kilikuwa kiovu machoni pa Mwenyezi Mungu, hivyo Mwenyezi Mungu akamuua Onani pia.
11Kisha Yuda akamwambia Tamari mkwewe, “Ishi kama mjane nyumbani mwa baba yako hadi mwanangu Shela atakapokua.” Kwa maana alifikiri, “Anaweza kufa pia kama ndugu zake.” Kwa hiyo Tamari akaenda kuishi nyumbani mwa baba yake.
12Baada ya muda mrefu, mke wa Yuda, binti Shua, akafariki. Baada ya msiba, Yuda alienda Timna kwa watu waliokuwa wakikata kondoo wake manyoya, naye alifuatana na rafiki yake Hira Mwadulami.
13Tamari alipoambiwa, “Baba mkwe wako yuko njiani akielekea Timna kukata kondoo wake manyoya,” 14alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike. Akaketi kwenye mlango wa Enaimu, njiani ya kuelekea Timna. Akafanya hivyo kwa sababu aliona kwamba ingawa Shela sasa alikuwa mtu mzima, bado hajakabidhiwa kwake kuwa mkewe.
15Yuda alipomwona alifikiri ni kahaba, kwa sababu alikuwa amefunika uso wake. 16Pasipo kutambua kwamba alikuwa mkwe wake, akamwendea kando ya njia na kumwambia, “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili.”
Yule mkwewe akamuuliza, “Utanipa nini nikikutana nawe kimwili?”
17Akamwambia, “Nitakutumia mwana-mbuzi kutoka kundi langu.”
Akamuuliza, “Utanipa amana hadi utakapompeleka?”
18Akamuuliza, “Nikupe amana gani?”
Akamjibu, “Pete yako na kamba yake pamoja na fimbo iliyo mkononi mwako.” Kwa hiyo akampa vitu hivyo, kisha akakutana naye kimwili, naye akapata mimba yake. 19Tamari akaondoka, akavua shela yake, akavaa tena nguo zake za ujane.
20Baadaye Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulami apeleke yule mwana-mbuzi ili arudishiwe amana yake kutoka kwa yule mwanamke, lakini yule rafiki yake hakumkuta yule mwanamke. 21Akawauliza watu walioishi mahali pale, “Yuko wapi yule kahaba wa mahali pa ibada za sanamu aliyekuwa kando ya barabara hapa Enaimu?”
Wakamjibu, “Hakujawahi kuwa kahaba wa mahali pa ibada za sanamu hapa.”
22Kwa hiyo akamrudia Yuda na kumwambia, “Sikumpata. Zaidi ya hayo, watu wanaoishi mahali pale walisema, ‘Hakujawahi kuwa kahaba wa mahali pa ibada za sanamu hapa.’ ”
23Kisha Yuda akasema, “Mwache avichukue vitu hivyo, ama sivyo tutaaibika. Hata hivyo, nilimpelekea mwana-mbuzi, lakini hukumkuta.”
24Baada ya miezi mitatu, Yuda akaambiwa, “Tamari mkweo ana hatia ya kuwa kahaba, na sasa ana mimba.”
Yuda akasema, “Mtoeni nje, achomwe moto hadi afe!”
25Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake kusema, “Nina mimba ya mtu mwenye vitu hivi.” Akaongeza kusema, “Angalia kama utatambua pete hii na kamba yake pamoja na fimbo hii ni vya nani.”
26Yuda akavitambua na kusema, “Yeye ana haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumkabidhi kwa mwanangu Shela ili awe mkewe.” Tangu hapo hakukutana naye kimwili tena.
27Wakati ulipofika wa kujifungua, kukawa na wana mapacha tumboni mwake. 28Alipokuwa akijifungua, mmoja akatoa mkono wake nje, kwa hiyo mkunga akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkononi mwa yule mtoto, akasema, “Huyu ametoka kwanza.” 29Lakini alipourudisha mkono wake, ndugu yake akatangulia kutoka, naye mkunga akasema, “Hivi ndivyo ulivyotoka kwa nguvu!” Akaitwa Peresi#38:29 maana yake Kutoka kwa nguvu. 30Kisha ndugu yake, aliyekuwa na uzi mwekundu mkononi, akatoka, naye akaitwa Zera#38:30 maana yake Wekundu au Kung’aa.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 38: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia