42
Ndugu za Yusufu waenda Misri
1Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka kule Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mkitazamana?” 2Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Teremkeni huko mkatununulie chakula, ili tuweze kuishi wala tusife.”
3Ndipo ndugu kumi wa Yusufu wakateremka huko Misri kununua nafaka. 4Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yusufu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara. 5Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale walioenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.
6Wakati huo Yusufu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, na ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yusufu walifika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi. 7Mara Yusufu alipowaona ndugu zake, akawatambua. Lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?”
Wakamjibu, “Tumetoka nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”
8Ingawa Yusufu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua. 9Ndipo Yusufu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.”
10Wakamjibu, “Sivyo, bwana. Watumishi wako wamekuja kununua chakula. 11Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
12Akawaambia, “La, hasha! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.”
13Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu, na mwingine alikufa.”
14Yusufu akawaambia, “Kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi! 15Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa hadi ndugu yenu mdogo aje hapa. 16Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu. Wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!” 17Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
18Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: 19Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. 20Lakini lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.
21Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuokoa maisha yake, lakini hatukumsikiliza. Hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”
22Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.” 23Hawakujua kuwa Yusufu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.
24Yusufu akajitenga nao, akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akaamuru Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.
25Yusufu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe chakula cha njiani. Baada ya kutendewa hayo yote, 26wakapakiza nafaka juu ya punda wao, wakaondoka.
27Walipofika mahali pa kulala huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake; akakuta fedha yake ndani ya gunia lake. 28Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.”
Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”
29Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema, 30“Huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi. 31Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. 32Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
33“Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu hapa kwangu, kisha nendeni mpeleke chakula kwa jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. 34Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu. Ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”
35Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, tazama! Wakapata ndani ya gunia la kila mtu mfuko wa fedha. Wakati wao na baba yao waliona mifuko ya fedha, wakaogopa. 36Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yusufu hayupo na Simeoni hayupo; tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”
37Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Unaweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”
38Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa, naye ndiye peke yake aliyebaki. Akipatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”