Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 2

2
Wokovu mkuu
1Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha. 2Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki, 3je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana Isa, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia. 4Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu, na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho wa Mungu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.
Isa alifananishwa na ndugu zake
5Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika. 6Lakini kuna mahali mtu mmoja ameshuhudia, akisema:
“Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,
binadamu ni nani hata unamjali?
7Umemfanya chini kidogo kuliko malaika;
ukamvika taji la utukufu na heshima,
8nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.”#2:8 Zaburi 8:4-6
Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake. 9Lakini twamwona Isa, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji la utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.
10Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kupitia kwa mateso yake. 11Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Isa haoni aibu kuwaita ndugu zake. 12Yeye anasema,
“Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu;
mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.”#2:12 Zaburi 22:22
13Tena,
“Nitaweka tumaini langu kwake.”#2:13 Isaya 8:17
Tena anasema,
“Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.”#2:13 Isaya 8:18
14Basi kwa kuwa watoto wana mwili na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, 15na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti. 16Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Ibrahimu. 17Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu. 18Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

Iliyochaguliwa sasa

Waebrania 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia