Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 9:1-8

Waebrania 9:1-8 NENO

Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi wa Utukufu, wakikitia kivuli kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kujadili vitu hivi kwa undani sasa. Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia mara kwa mara katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada. Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia. Kwa njia hii, Roho wa Mungu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa.