Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 9

9
Ibada katika hema la kidunia
1Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. 2Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. 3Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, 4ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. 5Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi wa Utukufu, wakikitia kivuli kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kujadili vitu hivi kwa undani sasa.
6Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia mara kwa mara katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada. 7Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia. 8Kwa njia hii, Roho wa Mungu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa. 9Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. 10Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.
Damu ya Al-Masihi
11Al-Masihi alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12Hakuingia kupitia kwa damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14Basi damu ya Al-Masihi, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, si itazisafisha dhamiri zetu zaidi kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!
15Kwa sababu hii Al-Masihi ni mpatanishi wa agano jipya, ili wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.
16Kwa habari ya wosia#9:16 yaani agano, ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa, 17kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu ameshakufa; kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika bado yuko hai. 18Hii ndiyo sababu hata lile agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu. 19Musa alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote. 20Alisema, “Hii ndiyo damu ya agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.”#9:20 Kutoka 24:8 21Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye ile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada. 22Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.
23Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. 24Kwa maana Al-Masihi hakuingia patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. 25Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe. 26Ingekuwa hivyo, ingempasa Al-Masihi kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu. 27Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28vivyo hivyo Al-Masihi alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

Iliyochaguliwa sasa

Waebrania 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia