Hosea 12:1-14
Hosea 12:1-14 NEN
Efraimu anajilisha upepo; hufukuzia upepo wa mashariki kutwa nzima na kuzidisha uongo na jeuri. Anafanya mkataba na Ashuru na kutuma mafuta ya zeituni Misri. BWANA analo shtaka dhidi ya Yuda, atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake na kumlipa kwa kadiri ya matendo yake. Yakobo akiwa tumboni alishika kisigino cha kaka yake; kama mwanadamu, alishindana na Mungu. Alishindana na malaika na kumshinda; alilia na kuomba upendeleo wake. Alimkuta huko Betheli na kuzungumza naye huko: BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, BWANA ndilo jina lake! Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako; dumisha upendo na haki, nawe umngojee Mungu wako siku zote. Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu; hupenda kupunja. Efraimu hujisifu akisema, “Mimi ni tajiri sana; nimetajirika. Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu uovu wowote au dhambi.” “Mimi ndimi BWANA Mungu wenu niliyewaleta kutoka Misri; nitawafanya mkae tena kwenye mahema, kama vile katika siku za sikukuu zenu zilizoamriwa. Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi na kusema mifano kupitia wao.” Je, Gileadi si mwovu? Watu wake hawafai kitu! Je, hawatoi dhabihu za mafahali huko Gilgali? Madhabahu zao zitakuwa kama malundo ya mawe katika shamba lililolimwa. Yakobo alikimbilia katika nchi ya Aramu; Israeli alitumika ili apate mke, ili aweze kulipa kwa ajili yake alichunga kondoo. BWANA alimtumia nabii kumpandisha Israeli kutoka Misri, kwa njia ya nabii alimtunza. Lakini Efraimu amemchochea sana hasira; Bwana wake ataleta juu yake hatia yake ya kumwaga damu naye atamlipiza kwa ajili ya dharau yake.