Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 13:1-11

Hosea 13:1-11 NEN

Wakati Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka, alikuwa ametukuzwa katika Israeli. Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali naye akafa. Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi; wanajitengenezea sanamu kutokana na fedha yao, vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari, vyote kazi ya fundi stadi. Inasemekana kuhusu hawa watu, “Hutoa dhabihu za binadamu na kubusu sanamu za ndama.” Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao, kama makapi yapeperushwayo kutoka sakafu ya kupuria nafaka, kama moshi utorokao kupitia dirishani. “Bali mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewaleta ninyi toka Misri. Msimkubali Mungu mwingine ila mimi, hakuna Mwokozi isipokuwa mimi. Niliwatunza huko jangwani, katika nchi yenye joto liunguzalo. Nilipowalisha, walishiba, waliposhiba, wakajivuna, kisha wakanisahau mimi. Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba, kama chui nitawavizia kando ya njia. Kama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, nitawashambulia na kurarua vifua vyenu. Kama simba nitawala; mnyama pori atawararua vipande vipande. “Ee Israeli, umeangamizwa, kwa sababu wewe u kinyume nami, kinyume na msaidizi wako. Yuko wapi mfalme wako, ili apate kukuokoa? Wako wapi watawala wako katika miji yako yote ambao ulisema kuwahusu, ‘Nipe mfalme na wakuu’? Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.