Hosea 14:4-9
Hosea 14:4-9 NEN
“Nitaponya ukaidi wao na kuwapenda kwa hiari yangu, kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; atachanua kama yungiyungi. Kama mwerezi wa Lebanoni atashusha mizizi yake chini; matawi yake yatatanda. Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni, harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni. Watu wataishi tena kwenye kivuli chake. Atastawi kama nafaka. Atachanua kama mzabibu, nao umaarufu wake utakuwa kama divai itokayo Lebanoni. Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu? Nitamjibu na kumtunza. Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi; kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.” Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya. Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa. Njia za BWANA ni adili; wenye haki huenda katika njia hizo, lakini waasi watajikwaa ndani yake.