Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 7:1-16

Hosea 7:1-16 NEN

kila mara nilipotaka kumponya Israeli, dhambi za Efraimu zinafichuliwa na maovu ya Samaria yanafunuliwa. Wanafanya udanganyifu, wevi huvunja nyumba, maharamia hunyangʼanya barabarani, lakini hawafahamu kwamba ninakumbuka matendo yao yote mabaya. Dhambi zao zimewameza, ziko mbele zangu siku zote. “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao, wakuu wao kwa uongo wao. Wote ni wazinzi, wanawaka kama tanuru ambayo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea kuanzia kukanda unga hadi umekwisha kuumuka. Katika sikukuu ya mfalme wetu wakuu wanawaka kwa mvinyo, naye anawaunga mkono wenye mizaha. Mioyo yao ni kama tanuru, wanamwendea kwa hila. Hasira yao inafoka moshi usiku kucha, wakati wa asubuhi inalipuka kama miali ya moto. Wote ni moto kama tanuru; wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wake wote wanaanguka, wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi. “Efraimu anajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate ambao haukuiva. Wageni wananyonya nguvu zake, lakini hafahamu hilo. Nywele zake zina mvi hapa na pale, lakini hana habari. Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake, lakini pamoja na haya yote harudi kwa BWANA Mungu wake wala kumtafuta. “Efraimu ni kama hua, hudanganywa kwa urahisi na hana akili: mara anaita Misri, mara anageukia Ashuru. Wakati watakapokwenda, nitatupa wavu wangu juu yao; nitawavuta chini waanguke kama ndege wa angani. Nitakaposikia wakikusanyika pamoja, nitawanasa. Ole wao, kwa sababu wamepotoka kutoka kwangu! Maangamizi ni yao kwa sababu wameniasi! Ninatamani kuwakomboa, lakini wanasema uongo dhidi yangu. Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao, bali wanaomboleza vitandani mwao. Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya, lakini hugeukia mbali nami. Niliwafundisha na kuwatia nguvu, lakini wanapanga mabaya dhidi yangu. Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana, wako kama upinde wenye kasoro. Viongozi wao wataanguka kwa upanga kwa sababu ya maneno yao ya jeuri. Kwa ajili ya hili watadhihakiwa katika nchi ya Misri.