Isaya 14:9-23
Isaya 14:9-23 NENO
Kuzimu kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa. Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.” Majivuno yako yote yameshushwa hadi Kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika. Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa! Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha utawala juu ya nyota za Mungu; nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu. Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.” Lakini umeshushwa chini hadi Kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo. Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke, yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa, aliyeipindua miji yake, na ambaye hakuwaachia mateka wake waende nyumbani?” Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake. Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako kama tawi lililokataliwa, umefunikwa na waliouawa pamoja na wale waliochomwa kwa upanga, wale wanaoshuka hadi kwenye mawe ya shimo. Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo, Hutajumuika nao kwenye mazishi, kwa kuwa umeharibu nchi yako na kuwaua watu wako. Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe. Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe kwa ajili ya dhambi za baba zao, wasije wakainuka ili kuirithi nchi na kuijaza dunia kwa miji yao. BWANA wa majeshi asema, “Nitainuka dhidi yao, nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika, watoto wake na wazao wake,” asema BWANA. “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi, na kuwa nchi ya matope; nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,” asema BWANA wa majeshi.