42
Mtumishi wa Mwenyezi Mungu
1“Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,
mteule wangu, ninayependezwa naye;
nitaweka Roho yangu juu yake,
naye ataleta haki kwa mataifa.
2Hatapaza sauti wala kupiga kelele,
wala hataipaza sauti yake barabarani.
3Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
na utambi unaofuka moshi hatauzima.
Kwa uaminifu ataleta haki,
4hatazimia roho wala kukata tamaa,
hadi atakaposimamisha haki juu ya dunia.
Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”
5Hili ndilo asemalo Mungu, Mwenyezi Mungu,
yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,
aliyeitandaza dunia na vyote vinavyotoka humo,
awapaye watu wake pumzi,
na uzima kwa wale wanaoenda humo:
6“Mimi, Mwenyezi Mungu, nimekuita katika haki;
nitakushika mkono wako.
Nitakulinda na kukufanya kuwa agano
kwa ajili ya watu
na nuru kwa Mataifa,
7kuwafungua macho wale wasioona,
kuwaacha huru kutoka kifungoni wale waliofungwa,
na kuwafungua kutoka gerezani
wale wanaokaa gizani.
8“Mimi ndimi Mwenyezi Mungu; hilo ndilo Jina langu!
Sitampa mwingine utukufu wangu
wala sanamu sifa zangu.
9Tazama, mambo ya kwanza yametokea,
nami natangaza mambo mapya;
kabla hayajatokea
nawatangazia habari zake.”
Wimbo wa kumsifu Mwenyezi Mungu
10Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo,
enyi visiwa na wote wanaoishi humo.
11Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;
makazi anamoishi Kedari na yashangilie.
Watu wa Sela waimbe kwa furaha,
na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
12Wampe Mwenyezi Mungu utukufu,
na kutangaza sifa zake katika visiwa.
13Mwenyezi Mungu ataenda kama mtu mwenye nguvu,
kama shujaa atachochea shauku yake,
kwa kishindo ataamsha ukelele wa vita,
naye atashinda adui zake.
14“Kwa muda mrefu nimenyamaza;
nimekaa kimya na kujizuia.
Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,
ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.
15Nitaharibu milima na vilima
na kukausha mimea yako yote;
nitafanya mito kuwa visiwa
na kukausha mabwawa.
16Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,
kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;
nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,
na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.
Haya ndio mambo nitakayofanya;
mimi sitawaacha.
17Lakini wale wanaotumaini sanamu,
wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’
watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.
Israeli ni kipofu na kiziwi
18“Sikieni, enyi viziwi;
tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!
19Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,
na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?
Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,
aliye kipofu kama mtumishi wa Mwenyezi Mungu?
20Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;
masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”
21Ilimpendeza Mwenyezi Mungu
kwa ajili ya haki yake
kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.
22Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,
wote wamenaswa katika mashimo,
au wamefichwa katika magereza.
Wamekuwa nyara,
wala hapana yeyote awaokoaye.
Wamefanywa mateka,
wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”
23Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili,
au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?
24Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,
na Israeli kwa wateka nyara?
Je, hakuwa yeye, Mwenyezi Mungu,
ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?
Kwa kuwa hawakufuata njia zake,
hawakutii sheria zake.
25Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,
ukali wa vita.
Iliwazunguka kwa miali ya moto,
lakini hata hivyo hawakuelewa;
iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.