44
Israeli aliyechaguliwa
1“Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Israeli, niliyemchagua.
2Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu,
yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,
yeye atakayekusaidia:
Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Yeshuruni#44:2 maana yake Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli, niliyekuchagua.
3Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu,
na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;
nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya watoto wako,
nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
4Nao watachipua kama nyasi katika shamba la majani,
kama mierezi kando ya vijito vya maji yanayotiririka.
5Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Mwenyezi Mungu’;
mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;
vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake,
‘Wa Mwenyezi Mungu,’
na kujiita kwa jina la Israeli.
Ni Mwenyezi Mungu, siyo sanamu
6“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu,
Mfalme wa Israeli na Mkombozi,
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;
zaidi yangu hakuna Mungu.
7Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.
Yeye atangaze na kuweka mbele yangu
ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,
tena ni nini kitakachotokea:
naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
8Msitetemeke, msiogope.
Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani?
Ninyi ni mashahidi wangu.
Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?
Hasha, hakuna Mwamba mwingine;
mimi simjui mwingine.”
9Wote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wanazitetea ni vipofu,
ni wajinga, nao waaibika.
10Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
12Muhunzi huchukua kifaa
na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,
hutengeneza sanamu kwa nyundo,
huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.
Huona njaa na kupoteza nguvu zake,
asipokunywa maji huzimia.
13Seremala hupima kwa kutumia kamba,
na huuchora mstari kwa kalamu;
huchonga kwa patasi
na kutia alama kwa bikari.
Huitengeneza katika umbo la binadamu,
umbo la binadamu katika utukufu wake wote,
ili iweze kukaa katika mahali pake pa ibada za sanamu.
14Hukata miti ya mierezi,
huchukua mtiriza au mwaloni.
Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,
au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
15Ni kuni ya binadamu:
yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,
huwasha moto na kuoka mkate.
Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,
huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16Sehemu ya kuni huziweka motoni,
akapikia chakula chake,
hubanika nyama na kula hadi ashibe.
Huota moto na kusema,
“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;
yeye huisujudia na kuiabudu.
Huiomba na kusema,
“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18Hawajui chochote, hawaelewi chochote,
macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,
akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
19Hakuna anayefikiri,
hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,
“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;
hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,
nikabanika nyama na kuila.
Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?
Je, nisujudie gogo la mti?”
20Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;
hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,
“Je, kitu hiki kilicho mkononi wangu wa kuume
si ni uongo?”
21“Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,
ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.
Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.
Ee Israeli, sitakusahau.
22Nimeyafuta makosa yako kama wingu,
dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.
Nirudie mimi,
kwa kuwa nimekukomboa wewe.”
23Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,
kwa maana Mwenyezi Mungu amefanya jambo hili.
Ee vilindi vya dunia, piga kelele.
Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,
enyi misitu na miti yenu yote,
kwa maana Mwenyezi Mungu amemkomboa Yakobo,
ameuonesha utukufu wake katika Israeli.
Yerusalemu itakaliwa
24“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu,
Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:
“Mimi ni Mwenyezi Mungu,
niliyeumba vitu vyote,
niliyezitanda mbingu peke yangu,
niliyeitandaza nchi mwenyewe.
25“Mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo,
na kuwatia upumbavu waaguzi,
niyapinduaye maarifa ya wenye hekima,
na kuyafanya kuwa upuzi.
26Mimi ndimi niyathibitishaye maneno ya watumishi wake,
na kutimiza utabiri wa wajumbe wake.
“Mimi ndiye niiambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’
niiambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’
na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’
27niiambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,
nami nitakausha vijito vyako,’
28nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,
naye atatimiza yote yanipendezayo;
atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”
na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’