62
Jina Jipya La Sayuni
1Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza,
kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,
mpaka haki yake itakapoangaza kama mapambazuko,
wokovu wake kama mwanga wa moto.
2 Mataifa wataona haki yako,
nao wafalme wote wataona utukufu wako;
wewe utaitwa kwa jina jipya
lile ambalo kinywa cha Bwana kitatamka.
3 Utakuwa taji ya fahari mkononi mwa Bwana,
taji ya kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4 Hawatakuita tena Aliyeachwa,
wala nchi yako kuiita Ukiwa.
Bali utaitwa Hefsiba,#62:4 Hefsiba maana yake Yeye ninayemfurahia.
nayo nchi yako itaitwa Beula,#62:4 Beula maana yake Aliyeolewa.
kwa maana Bwana atakufurahia,
nayo nchi yako itaolewa.
5 Kama vile kijana aoavyo mwanamwali,
ndivyo wanao#62:5 Au: wajenzi wako. watakavyokuoa wewe;
kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake,
ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu,
hawatanyamaza mchana wala usiku.
Ninyi wenye kumwita Bwana,
msitulie,
7 msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu
na kuufanya uwe sifa ya dunia.
8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume
na kwa mkono wake wenye nguvu:
“Kamwe sitawapa tena adui zenu
nafaka zenu kama chakula chao;
kamwe wageni hawatakunywa tena
divai mpya ambayo mmeitaabikia,
9lakini wale waivunao nafaka wataila
na kumsifu Bwana,
nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake
katika nyua za patakatifu pangu.”
10 Piteni, piteni katika malango!
Tengenezeni njia kwa ajili ya watu.
Jengeni, jengeni njia kuu!
Ondoeni mawe.
Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.
11 Bwana ametoa tangazo
mpaka miisho ya dunia:
“Mwambie Binti Sayuni,
‘Tazama, mwokozi wako anakuja!
Tazama ujira wake uko pamoja naye,
na malipo yake yanafuatana naye!’ ”
12 Wataitwa Watu Watakatifu,
Waliokombolewa na Bwana;
nawe utaitwa Aliyetafutwa,
Mji Usioachwa Tena.