20
Waisraeli wapigana na Wabenyamini
1Ndipo Waisraeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na wa kutoka nchi ya Gileadi wakatoka kama mtu mmoja, wakakusanyika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa. 2Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakakaa kwenye nafasi zao katika kusanyiko la watu wa Mungu, ambao walikuwa askari elfu mia nne walioenda kwa miguu wenye panga. 3(Wabenyamini wakasikia kuwa Waisraeli wamepanda kwenda Mispa.) Ndipo Waisraeli wakasema, “Tuelezeni jinsi jambo hili ovu lilivyotendeka.”
4Hivyo yule Mlawi, mume wa yule mwanamke aliyeuawa, akasema, “Mimi na suria wangu tulifika Gibea ya Benyamini ili tulale huko. 5Wakati wa usiku wanaume wa Gibea wakanijia na kuizingira nyumba, wakitaka kuniua. Wakambaka suria wangu hata akafa. 6Ndipo nikamchukua suria wangu, nikamkatakata vipande vipande na kuvipeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli, kwa kuwa wametenda uasherati mkubwa na jambo la aibu katika Israeli. 7Sasa, ninyi Waisraeli wote, semeni na mtoe uamuzi wenu.”
8Watu wote wakainuka wakasema, kama mtu mmoja, “Hakuna hata mmoja wetu atakayeenda nyumbani. Hakuna hata mmoja wetu atakayerudi nyumbani kwake. 9Sasa hili ndilo tutakaloitendea Gibea: Tutaikabili jinsi kura itakavyotuongoza. 10Tutatoa watu kumi katika kila mia moja kutoka kwenye makabila yote ya Israeli, watu mia moja katika kila elfu moja, na watu elfu moja katika kila elfu kumi, ili waende wakalete mahitaji kwa ajili ya jeshi. Basi wakati jeshi litakapofika Gibea ya Benyamini, watawatendea yale wanayostahili, kwa ajili ya uovu huu walioutenda katika Israeli.” 11Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakutanika pamoja na kujiunga kama mtu mmoja dhidi ya huo mji.
12Makabila ya Israeli yakatuma watu kwenda katika kabila la Benyamini lote na kuwaambia, “Ni uovu gani huu wa kutisha uliotendeka kati yenu? 13Basi watoeni hao wanaume waovu wa Gibea, ili tupate kuwaua na kuuondoa uovu katika Israeli.”
Lakini Wabenyamini hawakuwasikia ndugu zao, Waisraeli. 14Wakatoka katika miji yao, wakakutanika Gibea ili kupigana na Waisraeli. 15Siku ile Wabenyamini wakakusanya watu elfu ishirini na sita kutoka miji yao waliojifunga panga, mbali na hao vijana wenye uwezo mia saba kutoka wale walioishi Gibea. 16Miongoni mwa askari hao, palikuwa na askari mia saba waliochaguliwa waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja wao angetupa jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosa.
17Nao wanaume wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, wakakusanya wanaume elfu mia nne hodari wenye panga.
18Waisraeli wakapanda Betheli na kumuuliza Mungu, “Ni nani miongoni mwetu atakayetangulia mbele yetu ili kupigana na Wabenyamini?”
Mwenyezi Mungu akawajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia.”
19Kesho yake asubuhi, Waisraeli wakaamka na kupiga kambi karibu na Gibea. 20Waisraeli wakaondoka ili kupigana na Wabenyamini, nao Waisraeli wakachukua nafasi zao katika vita huko Gibea. 21Wabenyamini wakatoka Gibea na kuwaua Waisraeli elfu ishirini na mbili siku hiyo. 22Lakini Waisraeli wakatiana moyo kila mmoja na mwenzake, nao wakachukua tena nafasi zao katika vile vita mahali pale walipokuwa siku ya kwanza. 23Waisraeli wakapanda mbele za Mwenyezi Mungu na kulia mbele zake hadi jioni. Nao wakamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, tupande tena kupigana vita na Wabenyamini, ndugu zetu?”
Mwenyezi Mungu akajibu, “Pandeni mkapigane nao.”
24Ndipo Waisraeli wakawakaribia Wabenyamini siku ya pili. 25Wakati huu, Wabenyamini walipotoka Gibea ili kupigana na Waisraeli, wakawaua wanaume elfu kumi na nane wenye panga.
26Ndipo jeshi lote, na Waisraeli wote, wakapanda Betheli, na huko wakakaa mbele za Mwenyezi Mungu wakilia. Wakafunga siku hiyo hadi jioni na kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu. 27Nao Waisraeli wakauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu. (Katika siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwa huko, 28na Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anahudumu mbele za hilo Sanduku.) Wakauliza, “Je, tupande tena kwenda vitani kupigana na Wabenyamini, ndugu zetu, au la?”
Mwenyezi Mungu akajibu, “Nendeni, kwa kuwa kesho nitawatia mikononi mwenu.”
29Basi Waisraeli wakaweka waviziaji kuizunguka Gibea. 30Kisha Waisraeli wakapanda kupigana na Wabenyamini katika siku ya tatu na kuchukua nafasi zao dhidi ya Gibea kama walivyokuwa wamefanya hapo awali. 31Wabenyamini wakatoka ili kukabiliana na Waisraeli, ambao waliwavuta Wabenyamini watoke katika mji. Wakaanza kupigana na wakawaua watu wapatao thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika uwanja na katika njia kuu, moja iendayo Betheli na nyingine Gibea.
32Wabenyamini walipokuwa wakiambiana, “Wanapigwa mbele yetu kama hapo awali,” nao Waisraeli waliambiana, “Turudini nyuma ili tuwavute wauache mji, waende kuelekea barabarani.”
33Wanaume wote wa Israeli wakaondoka kwenye nafasi zao na kujipanga huko Baal-Tamari, nao wale waviziaji wa Waisraeli wakatoka ghafula walipokuwa kwenye uwanda wa magharibi mwa Gibea. 34Ndipo vijana wenye uwezo elfu kumi katika Israeli wakaja kuishambulia Gibea. Vita vilikuwa vikali sana, hata Wabenyamini hawakutambua kuwa maangamizi yalikuwa karibu nao. 35Mwenyezi Mungu akawashinda Wabenyamini mbele ya Waisraeli, na siku hiyo Waisraeli wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano na mia moja wenye panga. 36Hivyo Wabenyamini wakaona kuwa wameshindwa.
Basi Waisraeli walikuwa wamewaondokea Wabenyamini, kwa sababu Waisraeli waliwategemea hao waviziaji waliokuwa wamewaweka karibu na Gibea. 37Wale waviziaji wakafanya haraka kuingia Gibea, wakasambaa na kuwaua watu wote wa mji kwa upanga. 38Waisraeli walikuwa wamekubaliana na hao waviziaji kuwa wangesababisha wingu kubwa la moshi lipande kutoka huo mji, 39ndipo Waisraeli wangegeuka kupigana.
Wabenyamini walikuwa wameanza kuwapiga na kuwaua Waisraeli (wapatao thelathini), hivyo wakasema, “Hakika tunawashinda kama tulivyowashinda katika vita hapo awali.” 40Lakini nguzo ya moshi ilipoanza kupanda kutoka mji ule, Wabenyamini wakageuka, na tazama: katika mji mzima, moshi ulikuwa ukipaa angani. 41Ndipo Waisraeli wakawageukia, nao Wabenyamini wakatiwa hofu, kwa kuwa walitambua kwamba maafa yamewajia. 42Basi wakakimbia mbele ya Waisraeli kuelekea nyikani, lakini hawakuweza kukwepa vile vita. Nao Waisraeli waliotoka katika ile miji wakawaua huko. 43Wakawazingira Wabenyamini pande zote, wakawafuatia na kuwafikia karibu na Gibea upande wa mashariki. 44Wakaanguka Wabenyamini elfu kumi na nane, wote wapiganaji hodari. 45Walipogeuka na kukimbia kuelekea nyikani hata kufikia mwamba wa Rimoni, Waisraeli wakawaua watu elfu tano huko njiani. Wakawafuatia kwa karibu hadi Gidomu, na huko wakawaua wanaume wengine elfu mbili.
46Siku hiyo wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano wenye panga, wapiganaji hodari. 47Lakini watu mia sita wakakimbia kuelekea nyikani katika mwamba wa Rimoni, na kukaa huko muda wa miezi minne. 48Waisraeli wakarudi na kuwaua kwa upanga Wabenyamini wote, pamoja na wanyama na kila walichokipata. Pia kila mji waliouona wakauchoma kwa moto.