Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 13:4-15

Yohana 13:4-15 NEN

hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni. Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?” Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.” Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.” Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.” Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!” Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi. Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi.