Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 17:1-10

Yohana 17:1-10 NEN

Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo. “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao.