Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 19

19
Hotuba ya sita ya Ayubu
Ayubu anajibu: Najua Mkombozi wangu yu hai
1Ndipo Ayubu akajibu:
2“Je, mtaendelea kunitesa hadi lini,
na kuniponda kwa maneno yenu?
3Mara kumi hizi mmenishutumu;
bila aibu mnanishambulia.
4Kama ni kweli nimepotoka,
kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe.
5Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu,
na kutumia unyonge wangu dhidi yangu,
6basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya,
naye amekokota wavu wake kunizunguka.
7“Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu;
ingawa ninaomba msaada, hakuna haki.
8Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita;
ameyafunika mapito yangu na giza.
9Amenivua heshima yangu,
na kuniondolea taji kichwani pangu.
10Amenibomoa kila upande hadi nimeisha;
ameling’oa tegemeo langu kama mti.
11Hasira yake imewaka juu yangu;
amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake.
12Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu;
yamenizingira,
yamepiga kambi kulizunguka hema langu.
13“Amewatenga ndugu zangu mbali nami;
wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa.
14Watu wa jamaa zangu wameenda mbali;
rafiki zangu wamenisahau.
15Wageni wangu na wajakazi wangu wananiona kama mgeni;
wananitazama kama mgeni.
16Namwita mtumishi wangu, wala haitiki,
ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe.
17Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu;
nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe.
18Hata watoto wadogo hunidhihaki;
ninapojitokeza, hunifanyia mzaha.
19Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa;
wale ninaowapenda wamekuwa kinyume nami.
20Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu;
nimeponea nikiwa karibu kufa.
21“Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma,
kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga.
22Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo?
Hamtosheki kamwe na mwili wangu?
23“Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu,
laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu,
24kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma,
au kuyachonga juu ya mwamba milele!
25Ninajua kwamba Mkombozi#19:25 au Mtetezi wangu yu hai,
naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.
26Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa,
bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;
27mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe:
mimi, wala si mwingine.
Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!
28“Mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda,
maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’
29ninyi wenyewe uogopeni upanga,
kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga,
nanyi ndipo mtajua kuwa kuna hukumu.”

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 19: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia