27
Neno la mwisho la Ayubu kwa rafiki zake
1Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:
2“Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,
Mwenyezi ambaye amenifanya
nionje uchungu wa nafsi,
3kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,
nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,
4midomo yangu haitanena uovu,
wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.
5Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi;
hadi nife, sitakana uadilifu wangu.
6Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha;
dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.
7“Watesi wangu wawe kama waovu,
nao adui zangu wawe kama wasio haki!
8Kwa maana mtu asiyemcha Mungu
analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali,
Mungu anapouondoa uhai wake?
9Je, Mungu husikiliza kilio chake,
shida zimjiapo?
10Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi?
Je, atamwita Mungu nyakati zote?
11“Nitawafundisha kuhusu uweza wa Mungu;
njia za Mwenyezi sitazificha.
12Ninyi nyote mmeona hili wenyewe.
Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?
13“Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu,
urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi:
14Hata watoto wake wawe wengi kiasi gani,
fungu lao ni kuuawa kwa upanga;
wazao wake hawatakuwa kamwe
na chakula cha kuwatosha.
15Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao,
nao wajane wao hawatawaombolezea.
16Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi,
na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,
17yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba,
mwenye haki atayavaa,
naye asiye na hatia
ataigawanya fedha yake.
18Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui,
kama kibanda alichotengeneza mlinzi.
19Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho;
afunguapo macho yake, yote yametoweka.
20Vitisho humjia kama mafuriko;
dhoruba humkumba ghafula usiku.
21Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka;
humzoa kutoka mahali pake.
22Humvurumisha bila huruma,
huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.
23Upepo humpigia makofi kwa dharau,
na kumfukuza atoke mahali pake.”