32
Sehemu ya tatu: Mazungumzo ya Elihu
(Ayubu 32–37)
Elihu awakemea rafiki zake Ayubu
1Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe. 2Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu. 3Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu. 4Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu, kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye. 5Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.
6Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema:
“Mimi ni mdogo kwa umri,
nanyi ni wazee;
ndiyo sababu niliogopa,
sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.
7Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme,
nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’
8Lakini ni Roho iliyo ndani ya mwanadamu,
pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo ufahamu.
9Sio wazee peke yao walio na hekima,
sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa.
10“Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni;
mimi nami nitawaambia ninalolijua.
11Nilingojea mlipokuwa mnaongea,
nilizisikiliza hoja zenu;
mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,
12niliwasikiliza kwa makini.
Lakini hakuna hata mmoja wenu
aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa;
hakuna hata mmoja wenu
aliyeweza kujibu hoja zake.
13Msiseme, ‘Tumepata hekima;
Mungu na amthibitishe kuwa mwongo,
wala si mwanadamu.’
14Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu,
nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.
15“Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema;
maneno yamewaishia.
16Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya,
kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?
17Mimi nami nitakuwa na la kusema;
mimi nami nitasema lile nilijualo.
18Kwa kuwa nimejawa na maneno,
nayo Roho iliyo ndani yangu inanisukuma;
19ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai,
kama kiriba kipya cha divai kilicho karibu kupasuka.
20Ni lazima niseme ili niweze kutulia;
ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.
21Sitampendelea mtu yeyote,
wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote;
22kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza,
Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.