37
Elihu atukuza maajabu ya Mwenyezi Mungu
1“Kwa hili moyo wangu unatetemeka,
nao unaruka kutoka mahali pake.
2Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake,
sauti ya ngurumo inayotoka kinywani mwake.
3Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote
na kuupeleka hata miisho ya dunia.
4Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake;
Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari.
Wakati sauti yake inanguruma tena,
huuachilia umeme wake wa radi.
5Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu;
yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.
6Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’
nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’
7Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake,
yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.
8Wanyama hujificha;
hubakia kwenye mapango yao.
9Dhoruba hutoka katika chumba chake,
baridi hutoka katika upepo uendao kasi.
10Pumzi ya Mungu hutoa barafu,
eneo kubwa la maji huganda.
11Huyasheheneza mawingu kwa maji,
naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.
12Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,
juu ya uso wa dunia yote,
kufanya lolote ayaamuruyo.
13Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,
au kuinyeshea dunia yake na kuonesha upendo wake.
14“Ayubu, sikiliza hili;
nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.
15Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu,
na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?
16Je, unajua mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,
hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?
17Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako
wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,
18je, unaweza kuungana naye katika kuzitandaza anga,
zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?
19“Tuambieni yatupasayo kumwambia;
hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.
20Je, aambiwe kwamba nataka kuongea?
Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?
21Basi hakuna awezaye kulitazama jua,
jinsi linavyong’aa angani,
upepo ukishafagia mawingu.
22Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu;
Mungu huja katika utukufu wa kutisha.
23Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia,
naye ametukuzwa katika uweza;
katika hukumu zake na haki yake kuu,
hatadhulumu.
24Kwa hiyo wanadamu humwogopa,
kwa kuwa yeye hamstahi yeyote
anayejidhania kuwa ana hekima.”