3
Mataifa yahukumiwa
1“Katika siku hizo na wakati huo,
nitakaporejesha neema ya Yuda na Yerusalemu,
2nitayakusanya mataifa yote na kuyaleta
katika Bonde la Yehoshafati#3:2 Yehoshafati maana yake Mwenyezi Mungu huhukumu pia 3:12; hivyo maana yake ni Bonde la Hukumu ya Mwenyezi Mungu..
Hapo nitaingia kwenye hukumu dhidi yao
kuhusu urithi wangu, watu wangu Israeli,
kwa kuwa waliwatawanya watu wangu
miongoni mwa mataifa
na kuigawa nchi yangu.
3Waliwapigia kura watu wangu
na kuwauza wavulana ili kupata makahaba;
waliwauza wasichana
ili wapate kunywa mvinyo.
4“Sasa una nini dhidi yangu, ee Tiro na Sidoni, nanyi nchi zote za Ufilisti? Je, mnanilipiza kwa yale niliyoyafanya? Kama mnalipa, mimi nitalipiza juu ya vichwa vyenu kwa kasi na kwa haraka yale mliyoyatenda. 5Kwa kuwa mlichukua fedha na dhahabu yangu pia mkabeba hazina zangu nzuri sana mkapeleka kwenye mahekalu yenu. 6Mliwauza watu wa Yuda na Yerusalemu kwa Wayunani, ili mpate kuwapeleka mbali na nchi yao.
7“Tazama nitawaamsha kutoka zile sehemu mlizowauza, nami nitawalipiza juu ya vichwa vyenu kile mlichofanya. 8Nitawauza wana wenu wa kiume na wa kike kwa watu wa Yuda, nao watawauza kwa Waseba, taifa lililo mbali.” Mwenyezi Mungu amesema.
9Tangazeni hili miongoni mwa mataifa:
Jiandaeni kwa vita!
Amsha mashujaa!
Wapiganaji wote wasogee karibu na kushambulia.
10Majembe yenu yafueni yawe panga,
na miundu yenu ya kukatia iwe mikuki.
Aliye dhaifu na aseme,
“Mimi nina nguvu!”
11Njooni haraka, ninyi mataifa yote kutoka pande zote,
kusanyikeni huko.
Shusha mashujaa wako, Ee Mwenyezi Mungu!
12“Mataifa na yaamshwe;
na yasonge mbele kuelekea Bonde la Yehoshafati,
kwa kuwa nitaketi mahali pale
kuhukumu mataifa yote yaliyo kila upande.
13Tia mundu,
kwa kuwa mavuno yamekomaa.
Njooni, mkanyage zabibu,
kwa kuwa shinikizo la kukamulia zabibu limejaa
na mapipa yanafurika:
kwa kuwa uovu wao ni mkubwa!”
14Umati mkubwa, umati mkubwa
katika bonde la uamuzi!
Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu ni karibu
katika bonde la uamuzi.
15Jua na mwezi vitatiwa giza,
na nyota hazitatoa mwanga wake tena.
16Mwenyezi Mungu atanguruma kutoka Sayuni
na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu;
dunia na mbingu vitatikisika.
Lakini Mwenyezi Mungu atakuwa kimbilio la watu wake,
ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli.
Baraka kwa watu wa Mwenyezi Mungu
17“Ndipo mtajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
Yerusalemu utakuwa mtakatifu;
kamwe wageni hawatauvamia tena.
18“Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya,
na vilima vitatiririka maziwa;
mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji.
Chemchemi itatiririka kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu
na kunywesha Bonde la Shitimu#3:18 au Bonde la Migunga..
19Lakini Misri itakuwa ukiwa,
Edomu itakuwa jangwa tupu,
kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda,
ambao katika nchi yao
walimwaga damu isiyo na hatia.
20Yuda itakaliwa na watu milele
na Yerusalemu itadumu vizazi vyote.
21Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe,
nitasamehe.”
Mwenyezi Mungu anakaa Sayuni!