22
Makabila ya mashariki kurudi nyumbani
1Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, 2naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. 3Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyowapa. 4Sasa kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa ng’ambo ya Yordani. 5Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria ambazo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa: yaani kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.”
6Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani kwao. 7(Kwa nusu ya kabila la Manase, Musa alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi mwa Yordani pamoja na ndugu zao.) Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki, 8akisema, “Rudini nyumbani kwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia mavazi mengi; nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.”
9Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la Mwenyezi Mungu kupitia Musa.
10Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani. 11Waisraeli hao wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi karibu na Yordani kwenye upande wa Israeli, 12Waisraeli hao wengine walikusanyika huko Shilo ili wapigane nao.
13Kwa hiyo Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, aende katika nchi ya Gileadi kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase. 14Wakatuma viongozi kumi pamoja naye, mmoja kutoka kwa kila kabila la Israeli, kila mmoja akiwa kiongozi katika jamaa miongoni mwa koo za Israeli.
15Walipofika Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia: 16“Kusanyiko lote la Mwenyezi Mungu wasema hivi: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli jinsi hii? Mmewezaje kumwacha Mwenyezi Mungu na kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi? 17Je, dhambi ya Peori haikutosha? Hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hadi leo hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo! 18Je, sasa ndiyo mnamwacha Mwenyezi Mungu?
“ ‘Mkimwasi Mwenyezi Mungu leo, kesho atawakasirikia kusanyiko lote la Israeli. 19Ikiwa nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya Mwenyezi Mungu, mahali Maskani ya Mwenyezi Mungu ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya Mwenyezi Mungu wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu, isipokuwa madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. 20Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, je, ghadhabu haikuwapata kusanyiko lote la Israeli? Si yeye pekee aliyekufa kwa ajili ya dhambi yake.’ ”
21Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema: 22“Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa Mwenyezi Mungu, msituache hai siku hii ya leo. 23Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha Mwenyezi Mungu, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, Mwenyezi Mungu mwenyewe na atupatilize leo.
24“Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli? 25Mwenyezi Mungu ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa Mwenyezi Mungu.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha Mwenyezi Mungu.
26“Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’ 27Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu Mwenyezi Mungu katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika Mwenyezi Mungu.’
28“Nasi tulisema, ‘Wakati wowote wakituambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’
29“Hili jambo la kumwasi Mwenyezi Mungu na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, isipokuwa madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, iliyo mbele ya Maskani yake na liwe mbali nasi.”
30Kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko, hao wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika. 31Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa Mwenyezi Mungu katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli kutoka kwa mkono wa Mwenyezi Mungu.”
32Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, na viongozi wakarudi Kanaani kutoka mkutano wao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi, nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli. 33Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.
34Nao Wareubeni na Wagadi wakaita madhabahu hayo Edi#22:34 yaani Shahidi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.