Maombolezo 4:12-22
Maombolezo 4:12-22 NEN
Wafalme wa dunia hawakuamini, wala mtu yeyote wa duniani, kwamba adui na watesi wangeweza kuingia kwenye malango ya Yerusalemu. Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake, na maovu ya makuhani wake, waliomwaga ndani yake damu ya wenye haki. Sasa wanapapasa papasa barabarani kama watu ambao ni vipofu. Wamenajisiwa kabisa kwa damu, hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao. Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi! Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!” Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko, watu miongoni mwa mataifa wanasema, “Hawawezi kukaa hapa zaidi.” BWANA mwenyewe amewatawanya; hawaangalii tena. Makuhani hawaonyeshwi heshima, wazee hawakubaliki. Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka, kwa kutazamia bure msaada; tuliangalia kutoka minara yetu kwa taifa lisiloweza kutuokoa. Watu walituvizia katika kila hatua hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu. Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia, kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika. Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai angani; walitusaka juu milimani na kutuvizia jangwani. Mpakwa mafuta wa BWANA, pumzi ya uhai wetu hasa, alinaswa katika mitego yao. Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa. Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu, wewe unayeishi nchi ya Usi. Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa, Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi. Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha, hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni. Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako, na atafunua uovu wako.