Luka 18:35-43
Luka 18:35-43 NEN
Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?” Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.” Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!” Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!” Yesu akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Yesu akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Akajibu, “Bwana, nataka kuona.” Yesu akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.” Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.