Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:40-65

Luka 22:40-65 NENO

Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.” Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini. Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.” Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu wakaja. Waliongozwa na Yuda, aliyekuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu. Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?” Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?” Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume. Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya. Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? Kila siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!” Kisha wakamkamata Isa, wakamchukua, wakaenda naye hadi nyumbani mwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali. Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao. Mjakazi mmoja akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Isa!” Lakini Petro akakana, akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!” Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!” Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Isa, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika. Naye Bwana Isa akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana alimwambia: “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi. Watu waliokuwa wanamlinda Isa wakaanza kumdhihaki na kumpiga. Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?” Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.