Luka 22:7-23
Luka 22:7-23 NENO
Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Isa akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.” Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?” Isa akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni hadi kwenye nyumba atakayoingia. Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ Atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.” Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka. Wakati ulipowadia, Isa akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka hadi itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.” Baada ya kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi ufalme wa Mungu utakapokuja.” Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu. Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye!” Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.