Luka 24:1-50
Luka 24:1-50 NENO
Siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini. Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka mdomo wa kaburi, lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Isa. Walipokuwa wanashangaa kuhusu jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayong’aa kama umeme wakasimama karibu nao. Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao hadi chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” Ndipo wakayakumbuka maneno ya Isa. Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. Basi Mariamu Magdalene, Yoana, na Mariamu mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi. Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi. Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea. Ikawa siku hiyo hiyo, wanafunzi wawili wa Isa walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba kutoka Yerusalemu. Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Isa mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue. Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?” Wakasimama, nyuso zao zikionesha huzuni. Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiwe peke yako mgeni huku Yerusalemu, ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?” Akawauliza, “Mambo gani?” Wakamjibu, “Mambo ya Isa Al-Nasiri. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatendeke. Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walienda kaburini leo alfajiri, lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Isa yu hai. Kisha baadhi ya wenzetu walienda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.” Isa akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! Je, haikumpasa Al-Masihi kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” Naye akianzia na Torati ya Musa na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu. Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Isa akawa kama anaendelea mbele. Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao. Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?” Wakaondoka mara hiyo, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao wamekusanyika, wakasema, “Ni kweli! Bwana Isa amefufuka, naye amemtokea Simoni.” Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Isa alipoumega mkate. Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Isa mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. Lakini Isa akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi mwenyewe. Niguseni mwone; kwa maana mzuka huna nyama na mifupa, kama mnavyoniona mimi.” Aliposema haya, akawaonesha mikono na miguu yake. Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, naye akakichukua na kukila mbele yao. Akawaambia, “Haya ndio yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu katika Torati ya Musa, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.” Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Haya ndio yaliyoandikwa: Al-Masihi atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. Ninyi ni mashahidi wa mambo haya. “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo kutoka juu.” Baada ya kuwaongoza hadi Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki.