Luka 9:28-36
Luka 9:28-36 NEN
Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana, akaenda nao mlimani kuomba. Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikabadilika, nayo mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi. Ghafula wakawaona watu wawili, ndio Mose na Eliya, wakizungumza naye. Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu. Petro na wenzake walikuwa wamelala usingizi mzito. Walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. Mose na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho. Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu, likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu. Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, niliyemchagua. Msikieni yeye.” Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu yeyote yale waliyokuwa wameyaona.