1
1Neno la unabii: Neno la Mwenyezi Mungu kwa Israeli kupitia kwa Malaki.
Yakobo alipendwa, Esau alichukiwa
2Mwenyezi Mungu asema, “Nimewapenda ninyi.
“Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ”
Mwenyezi Mungu asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo, 3lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya nchi yake ya vilima kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.”
4Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondapondwa, tutajenga upya magofu.”
Lakini hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. 5Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi Mungu ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’
Dhabihu zilizo na mawaa
6“Mwana humheshimu baba yake, naye mtumishi humheshimu bwana wake. Kama mimi ni baba, iko wapi heshima ninayostahili? Kama mimi ni bwana, iko wapi heshima ninayostahili?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Ni ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau Jina langu.
“Lakini mnauliza, ‘Tumelidharau Jina lako kwa namna gani?’
7“Mnatoa sadaka chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu.
“Lakini ninyi mnauliza, ‘Tumekutia unajisi kwa namna gani?’
“Kwa kusema kuwa meza ya Mwenyezi Mungu ni ya kudharauliwa. 8Mnapoleta dhabihu za wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahishwa nanyi? Je, atawakubalia?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
9“Basi mwombeni Mungu awe na neema kwetu. Je, kwa sadaka kama hizo kutoka mikononi mwenu, atawapokea?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
10“Laiti mmoja wenu angeifunga milango ya Hekalu, ili msije mkawasha moto usiokuwa na faida juu ya madhabahu yangu! Sina furaha nanyi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “nami sitaikubali sadaka toka mikononi mwenu. 11Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa, kuanzia mawio ya jua hata machweo yake. Kila mahali uvumba na sadaka safi zitaletwa kwa Jina langu, kwa sababu Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
12“Lakini mnalinajisi Jina langu kwa kusema kuhusu meza ya Bwana, ‘Imetiwa unajisi pamoja na chakula chake. Ni ya kudharauliwa.’ 13Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
“Mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, walio vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema Mwenyezi Mungu. 14“Amelaaniwa yeye adanganyaye, aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.