Malaki 3:6-12
Malaki 3:6-12 NENO
“Mimi Mwenyezi Mungu sibadiliki. Kwa hiyo ninyi, enyi uzao wa Yakobo, hamjaangamizwa. Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’ “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi. “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’ “Mnaniibia zaka na dhabihu. Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi hata mkose nafasi ya kutosha. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.