12
Isa ni Bwana wa Sabato
(Marko 2:23-28; Luka 6:1-5)
1Wakati huo Isa alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. 2Lakini Mafarisayo#12:2 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”
3Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? 4Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu. 5Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. 7Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’#12:7 Hosea 6:6 msingewalaumu watu wasio na hatia, 8kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
Isa amponya mtu aliyepooza mkono
(Marko 3:1-6; Luka 6:6-11)
9Isa akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi#12:9 Nyumba ya ibada na mafunzo. lao, 10na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11Isa akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? 12Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
13Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. 14Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Isa.
Mtumishi aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu
15Lakini Isa alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao, 16akiwakataza wasiseme yeye ni nani, 17ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema:
18“Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Nitaweka Roho wangu Mtakatifu juu yake,
naye atatangaza haki kwa mataifa.
19Hatagombana wala kupaza sauti,
wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
20Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
na utambi unaofuka moshi hatauzima,
hadi atakapoifanya haki ishinde.
21Katika Jina lake mataifa
wataweka tumaini lao.”#12:21 Isaya 42:1-4
Isa na Beelzebuli
(Marko 3:20-30; Luka 11:14-23)
22Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Isa akamponya, hata akaweza kusema na kuona. 23Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi#12:23 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4).?”
24Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli#12:24 au Beelzebubu; pia 12:27, mkuu wa pepo wachafu.”
25Isa alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
29“Au tena, mtu anawezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali yake.
30“Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. 31Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa. 32Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho wa Mungu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.
Mti na matunda yake
(Luka 6:43-45)
33“Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. 34Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. 36Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa maelezo kuhusu kila neno walilonena lisilo la maana. 37Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
Ishara ya Yona
(Marko 8:11-13; Luka 11:29-32)
38Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Torati wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
39Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa sana kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Sulemani. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
Mafundisho kuhusu pepo mchafu
(Luka 11:24-26)
43“Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. 44Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye anaporudi huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. 45Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”
Mama yake na ndugu zake Isa
(Marko 3:31-35; Luka 8:19-21)
46Wakati alikuwa angali anazungumza na umati wa watu, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye. 47Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”
48Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” 49Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu! 50Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba#12:50 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu wa mbinguni, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”