15
Mapokeo Ya Wazee
(Marko 7:1-13)
1 Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjia Yesu kutoka Yerusalemu na kumuuliza, 2 “Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”
3Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? 4 Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 5 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ 6basi hana tena sababu ya kumheshimu baba yake nacho. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu. 7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:
8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
9 Huniabudu bure;
nayo mafundisho yao
ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”
Vitu Vitiavyo Unajisi
(Marko 7:14-23)
10 Yesu akaita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe: 11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”
12Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”
13 Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litangʼolewa. 14 Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”
16 Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
Imani Ya Mwanamke Mkanaani
(Marko 7:24-30)
21 Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”
23Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”
24 Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”
25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”
26Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
27Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”
28 Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.
Yesu Aponya Watu Wengi
29Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. 30 Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. 31 Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.
Yesu Alisha Watu Elfu Nne
(Marko 8:1-10)
32 Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”
33Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”
34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”
35Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. 36 Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. 37 Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 38Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.#15:39 Magadani ni Magdala, mji wa Galilaya, kama kilomita 16 kusini mwa Kapernaumu.